top of page

Mwongozo wa Kujiandaa na Ibada ya Umrah

Utangulizi

Awali ya yote, ninamshukuru Allaah A’zza wa Jall[1] kwa kuweza kunipa uwezo kuandika machache kuhusu Ibada ya Umra. Ibada ambayo ni Sunnah iliyokokotezwa (na baadhi ya maulamaa wamesema ni wajibu) kwa kila Muislamu mwenye uwezo.

Pia Rehma na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) pamoja na Masahaba zake, Taabiina na wote waliofuata uongofu kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم).

Ndugu yangu katika Imani unayetarajia kuitekeleza Ibada muhimu ya Umra. Mwongozo ni kitu muhimu katika kila jambo. Kiongozi wa Umra, ambaye ni wajibu wetu kumfuata, ni Mtume Muhammad (صلى الله عليه وسلم).

Imebainika kutokana na uzoefu kwamba ni vigumu sana kwa kila mwenye kutaka kuitekeleza ibada ya Umra, kuweza kukumbuka kila kinachohitajiwa katika kuitekeleza amali hii, hivyo ukiwa na mwongozo, utaweza kukusaidia wakati utakapotekeleza ibada hii.

Ndugu yangu katika Imani, kitabu hiki ni kidogo tu na kimeandikwa kwa lugha nyepesi kumrahisishia mwenye kuitekeleza Ibada hii ya Umra kuifahamu kirahisi na kuweza kumpa mwongozo kila mwenye kutaka kutekeleza ibada hii na kumrahisishia wakati wa kuitekeleza.

Kimekusanya mambo mengi ya kimsingi ambayo yanahusiana Umra pamoja na kufanya ziara katika Msikiti wa Mtume (صلى الله عليه وسلم), Madina.

Kitabu kimejitahidi kuleta ushahidi wa Qur’aan na Sunnah katika kuhakikisha kila jambo linalofanyika lina ushahidi kwa kadri ya Allaah A’zza wa Jall alivyotujaalia.

Mwongozo huu utumike kwa yule ambae anataka kuitekeleza ibada ya Umra pekee na si katika wakati wa msimu wa Hijja.[2]

Ninamuomba Allaah A’zza wa Jall aijaalie amali hii ndogo iwe ni kwa ajili ya kupata radhi zake na iwanufaishe watakaojaaliwa kukisoma, pia iwaongoze watakaojaaliwa kuzitekeleza ibada hizi, bi idhni Llaah, Ibada yao ya Umra iwe maqbuul (itakabaliwe) na dhambi zao ziwe maghfuur (zisamehewe) na Sa’iy zao ziwe Mashkuur (zenye kushukuriwa). Aamin.

 

[1] Mwenye nguvu na Mshindi

[2] Ama yule mwenye kutaka kuitekeleza ibada hii katika msimu wa Hijja akitafute kitabu chengine cha ‘Mwongozo wa kuzitekeleza Ibada za Hijja na Umra’

  • Facebook
  • Twitter
  • LinkedIn
  • Instagram
bottom of page