رب يسر ولا تعسر
Utangulizi wa Mfasiri
Himdi zote ni za Allah, tunamshukuru Yeye, na tunamtaka msaada, na tunamuomba Atuhidi, na tunatubia Kwake kwa dhambi na makosa yetu yote; na pia tunaomba hifadhi Kwake Allah kutokana na shari za (maovu ya) nafsi zetu, na ubaya wa amali zetu; yeyote yule ambae Allah Amemhidi, basi huwa hakuna wa kumpoteza, na yeyote yule aliyepotea, huwa hakuna wa kumhidi na wala hakuna uwezekano wa kumpatia msaidizi wa kumuongoza.
Nashuhudia kwamba hakuna Ilahi Apaswae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, Mmoja Pekee, Ambae Hakuzaa wala Hakuzaliwa, na wala Hana mshirika yoyote yule; na ninashuhudia kuwa Nabii Muhammad ﷺ ni Mja Wake na ni Rasuli Wake wa mwisho; Rehema na Amani za Allah zimshukie yeye na wake zake na dhuria wake na jamaa zake, na Swahaba zake (Allah Awe Radhi Nao Jamia), na kila anayewafuata kwa ihsani mpaka Siku ya Qiyamah .
Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿ ﴾١٠٢
“Enyi mlioamini! Muogopeni Allah vile Apasavyo kuogopwa; na wala msife isipokuwa na nyinyi ni Waislamu” , pia Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١﴾
“Enyi watu! Mcheni Rabi wenu Ambae Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Adam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawa) na Akaeneza kutoka wawili hao wanaume wengi na wanawake (wengi pia); na mcheni Allah Ambae Kwake mnaombana na jamaa; hakika Allah Amekuwa juu yenu Raqiba (Mwenye kuchunga)” , pia Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
“Enyi mlioamini! Mcheni Allah, na semeni kauli ya kweli (ya sawasawa); Atakutengenezeeni amali zenu, na Atakughufurieni dhambi zenu; na yeyote yule anayemtii Allah na Rasuli Wake ﷺ, basi amekwishafanikiwa mafanikio adhimu” .
Ama baada ya hayo! Kwa hakika, Hadithi iliyo nzuri kabisa ni Kitabu cha Allah, na uongofu ulio mzuri (bora) kabisa ni uongofu wa Nabii Muhammad ﷺ; na shari ya mambo yote ni yale mambo ya kuzushwa, na kila jambo la kuzushwa ni bidaa , na kila bidaa ni dhalala (upotevu).
Namshukuru Allah kwa kuniwafikisha kuweza kukamilisha kazi hii ya kufasiri kijitabu hichi, kazi ninayoamini kuwa ni miongoni mwa juhudi zinazolengwa kwa gharadhi ya kutumikia na kuhudumia Dini, kazi ambayo ninaamini kuwa itawanufaisha Waislamu wenzangu wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili (hasahasa ahali wa darsa na mihadhara) kwa kuwafikishwa kuweza kuelewa karibu yale yote yenye kuhusiana na Siku Kumi za mwanzo za shahari ya Dhul Hijjah.
Kwa kweli kazi mithili ya hii na nyengine nyingi mithili yake ni changamoto miongoni mwa changamoto zinazokabili ummah kwa gharadhi ya kushajiisha wanaharakati na wenye kujinasibisha na ahali wa Sunnah hususan kutoa michango yao iwe kwa kufasiri, au kuandika, au kudarasisha, au kuhadhiri na kadhalika; michango itayoweza kufikia kusahihisha, au kurekebisha, au kusawazisha pale panapoonekanwa kuwa panatakikana hayo katika jamii yetu.
Kwa mintarafu hiyo basi, nimeona kuwa kuna haja na umuhimu wa kufasiri kijitabu hichi –Fadhila za Siku Kumi za Dhul Hijjah فضل أيام عشر ذي الحجة – cha Shaykh na mwanachuoni Ibn Uthaymini (Rahimahullahu) chenye ushauri, maelezo, tahadhari, mapendekezo na ufafanuzi wake (Rahimahullahu) wenye kuhusiana na mada husika.
Akh wangu katika imani -Allah Akurehemu- tumia wakati wako adhimu upate kufaidika kutakoweza kukufikisha na kukupelekea kujihimu na kuchangamka katika kutenda amali njema katika haya masiku kumi ya mwanzo ya Dhul Hijjah amali zitazokuwa na maslahi na faida kwako huko Akhera kwa kuwa ni amali zinazopendwa mno na Allah kwa sababu ulizitenda katika haya masiku kumi ya Dhul Hijjah.
Namuomba Allah Ajaaliye kazi hii iwe yenye ikhlasi kwa kutafuta Wajihi Wake; na Awalipe wale wote waliopelekea kukamilika kwa kazi hii (hususan ahali wa darsa na mihadhara, na bila ya kumsahau mhadhiri wetu Ust. Salim Khatib Hafidhahullahu kutoka Barking UK na wengineo) kila la heri hapa duniani na huko Akhera.
Allaahuma Aamin.
Wakatabahu: Abu Farouq
Dhul Hijjah 1445 – Juni 2024
Utangulizi wa Mwandishi
الحمد لله ربّ العالمين، والصلاة والسلام على سيد المرسلين وبعد..
Alhamdulillahi Rabbil ‘alamina (Himda zote ni za Allah Rabbi wa walimwengu); na Sala na Salamu zimshukie Sayyidil Mur-salina (Muhammad ﷺ).
Nashuhudia kwamba hakuna ilahi Apaswae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, Mmoja Pekee, Ambae Hakuzaa wala Hakuzaliwa, na wala Hana mshirika yoyote yule; na ninashuhudia kuwa Nabii Muhammad ﷺ ni Mja Wake na ni Rasuli Wake wa mwisho; Rehema na Amani za Allah zimshukie yeye na wake zake na dhuria wake na jamaa zake, na Swahaba zake (Allah Awe Radhi Nao Jamia), na kila anayewafuata kwa ihsani mpaka Siku ya Qiyamah.
Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٢
﴾“Enyi mlioamini! Muogopeni Allah vile Apasavyo kuogopwa; na wala msife isipokuwa na nyinyi ni Waislamu” ,
Pia Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا ﴿١
﴾“Enyi watu! Mcheni Rabi wenu Ambae Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Adam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawa) na Akaeneza kutoka wawili hao wanaume wengi na wanawake (wengi pia); na mcheni Allah Ambae Kwake mnaombana na jamaa; hakika Allah Amekuwa juu yenu Raqiba (Mwenye kuchunga)” ,
Pia Allah Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾ يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١
﴾“Enyi mlioamini! Mcheni Allah, na semeni kauli ya kweli (ya sawasawa); Atakutengenezeeni amali zenu, na Atakughufurieni dhambi zenu; na yeyote yule anayemtii Allah na Rasuli Wake ﷺ, basi amekwishafanikiwa mafanikio adhimu” .
Baada ya hayo ….,
kwa hakika miongoni mwa Fadhila za Allah na Ihsani Zake kwamba Amewawekea Waja Wake wema misimu ili wapate ndani yake kukithirisha utendaji na utekelezaji wa amali njema, na miongoni mwa hiyo misimu ni huu msimu wa Siku kumi za Dhul Hijjah.
Fadhila za Siku Kumi za (mwanzo za) Dhul Hijjah
فضل عشر ذي الحجة
Kwa hakika kuhusiana na fadhila zake, kumepokelewa dalilli nyingi kutoka kwenye Kitabu (Qur aani) na Sunnah, miongoni mwake ni:
1.Kauli Yake Ta’alaa:
وَالْفَجْرِ ﴿١﴾ وَلَيَالٍ عَشْرٍ ﴿٢
﴾“(Naapa kwa Al Fajri). Na kwa masiku kumi.”
Ibn Kathir (Rahimahullahu) amesema kuwa: ‘Muradi wake (kinachokusudiwa) ni siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah, kama walivyosema hivyo kina Ibn Abbas (Allah Awe Radhi Nao), na Ibnuz Zubeir (Allah Awe Radhi Nae), na Mujahid (Rahimahullahu) na wengineo’, na amepokea hayo imamu Bukhari (Rahimahullahu).
2.Kauli ya Rasuli wa Allah
ﷺ:عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ " مَا مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ هَذِهِ الأَيَّامِ "
. يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ . قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ وَلاَ الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ قَالَ " وَلاَ الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلاَّ رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَىْءٍ " .
Kutokana na Ibn Abbas (Allah Awe Radhi Nao) amesema kuwa Rasuli wa Allah ﷺ amesema: “Hakuna siku ambazo amali njema (zinazotendwa) ndani yake huwa zinapendeza mno kwa Allah kuliko (zile amali zinazotendwa katika) hizi siku kumi.” Yaani: Siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah.” (Swahaba Allah Awe Radhi Nao Jamia) wakauliza kwa kusema: ‘Ewe Rasuli wa Allah ﷺ! Hata kuliko Jihadi katika Sabili ya Allah? Rasuli wa Allah ﷺ akawajibu kwa kusema: “Hata Jihadi katika Sabili ya Allah isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda Jihadi) kwa nafsi yake na mali yake kisha kisirudi chochote kile katika hivyo.”
3.Kauli Yake Ta’alaa:
وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ .. ﴿٢٨
﴾“Na wadhukuru (wataje) Jina la Allah katika masiku yanayojulikana….”
Ibn Abbas (Allah Awe Radhi Nao) na Ibn Kathir (Rahimahullahu) wamesema: ‘Yaani: Siku kumi za Dhul Hijjah.’
4.Kauli ya Rasuli wa Allah
ﷺ:عن ابن عمر رضي الله عنهما عن النبي ﷺ قال” ما من أيام أَعْظَمُ عند الله ولا أَحَبُّ إليه العمل فيهن من هذه الأيام العشر :فأكثروا فيهن من التهليل والتكبير والتحميد".
Kutokana na Ibn Umar (Allah Awe Radhi Nao) kutokana na Nabii ﷺ kuwa amesema: "Hakuna siku zilizo adhimu zaidi mbele ya Allah na wala hakuna amali Anayoipenda mno (kufanywa) ndani yake kuliko siku hizi kumi (yaani: siku kumi za mwanzo za Dhul Hijjah); basi kithirisheni ndani yake Tahlili, na Takbiri, na Tahmidi.”
5.Said bin Jubair (Rahimahullahu) - ambae ndie aliyepokea Hadithi ya Ibn Abbas Allah Awe Radhi Nao- alikuwa pale zinapowadia siku kumi za Dhul Hijjah hujitahidi jitihada ya kipekee mpaka anafikia kutoweza kuhimili.
6.Na Ibn Hajar (Rahimahullahu) katika (Fat-h) amesema kuwa: 'Na kile ambacho kinadhihiri kuwa ndio sababu ya kujinyakulia heshina na upendeleo hizi siku kumi za Dhul Hijjah ni kwa kule kukusanyika na kujumuika ndani yake ummahaati (mama) wa ibada zote; Sala, na Saumu, na Sadaka na Hija, na wala hazikusanyiki pamoja wakati mwengine wowote ule.
ما يستحب فعله في هذه الأيام
Yenye Kupendeza Kufanywa Katika Siku Kumi Hizi
1.Sala:
Itapendeza kwa mja kuwahi mapema kwenda (masjidi) kusali Sala za fardhi, na (pia itapendeza) kukithirisha kusali Nawaafil (Sala za Sunnah) kwa kuwa ni Qurubaati (kurubisho: yaani lenye kumkurubisha mja zaidi kwa Rabi wake) lililobora zaidi.
عَنْ مَعْدَانُ بْنُ أَبِي طَلْحَةَ الْيَعْمَرِيُّ، قَالَ لَقِيتُ ثَوْبَانَ مَوْلَى رَسُولِ اللَّهِ ﷺ فَقُلْتُ أَخْبِرْنِي بِعَمَلٍ أَعْمَلُهُ يُدْخِلُنِي اللَّهُ بِهِ الْجَنَّةَ . أَوْ قَالَ قُلْتُ بِأَحَبِّ الأَعْمَالِ إِلَى اللَّهِ . فَسَكَتَ ثُمَّ سَأَلْتُهُ فَسَكَتَ ثُمَّ سَأَلْتُهُ الثَّالِثَةَ فَقَالَ سَأَلْتُ عَنْ ذَلِكَ رَسُولَ اللَّهِ ﷺ فَقَالَ " عَلَيْكَ بِكَثْرَةِ السُّجُودِ لِلَّهِ فَإِنَّكَ لاَ تَسْجُدُ لِلَّهِ سَجْدَةً إِلاَّ رَفَعَكَ اللَّهُ بِهَا دَرَجَةً وَحَطَّ عَنْكَ بِهَا خَطِيئَةً
"Kutokana na Ma'daan bin Abu Twalha Al Ya’mariyu amesema: 'Nilikutana na Thaubana maula (muachwa huwa) wa Rasuli wa Allah ﷺ nikamwambia: Nieleze amali ambayo Allah Atanitunuku (Ataniingiza) kwayo Jannah?’ Au amesema: 'Nieleze amali inayopendeza zaidi mbele ya Allah?’ Basi alinyamaza, kisha nikamuuliza (tena kwa mara ya pili) alinyamaza (pia), na kisha nikamuuliza (tena kwa) mara ya tatu; ndipo aliponijibu kwa kusema: ‘Nilimuuliza Rasuli wa Allah ﷺ kuhusiana na hilo, basi Rasuli wa Allah ﷺ alinijibu kwa kusema: “Kithirisha kumsujudia Allah, kwani hakika hutomsujudia Allah sijida isipokuwa Allah Atakunyanyuwa kwayo daraja, na Atakuondoshea kwayo dhambi.” Na hii ni jumla ni katika nyakati zote.
2.Saumu: Kwa kule kuingia kwake katika amali njema
عَنْ هُنَيْدَةَ بْنِ خَالِدٍ عَنِ امْرَأَتِهِ عَنْ بَعْضِ أَزْوَاجِ النَّبِيِّ ﷺ قَالَتْ: كَانَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ يَصُومُ تِسْعَ ذِي الْحِجَّةِ وَيَوْمَ عَاشُورَاءَ وَثَلاَثَةَ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ أَوَّلَ اثْنَيْنِ مِنَ الشَّهْرِ وَالْخَمِيسَ .
Kutokana na Hunaydah ibn Khalid kutokana na mkewe kutokana na baadhi ya wake wa Nabii ﷺ amesema kuwa: 'Alikuwa Rasuli wa Allah ﷺ akifunga siku tisa za (mwanzo za) Dhul Hijjah, na (pia alikuwa akifunga) Siku ya Ashuraa, na (pia alikuwa akifunga) siku tatu katika kila shahari, yaani, Jumatatu ya kwanza (ya mwezi) na Alhamisi.”
Kuhusiana na kufunga siku kumi, imamu Nawawi (Rahimahullahu) amesema kuwa ni: ' Mustahabbu (kunapendeza) mpendezo shadidi.'
3. (Kukithirisha kuleta) Takbiri na Tahlili, na Tahmidi.
Kutokana na kile kilichokuja katika Hadithi ya Ibn Umar (Allah Awe Radhi Nao) iliyotangulia:
"فأكثروا فيهن من التهليل والتكبير والتحميد".
"Basi kithirisheni ndani yake Tahlili, na Takbiri, na Tahmidi.
” وَكَانَ ابْنُ عُمَرَ وَأَبُو هُرَيْرَةَ يَخْرُجَانِ إِلَى السُّوقِ فِي أَيَّامِ الْعَشْرِ يُكَبِّرَانِ، وَيُكَبِّرُ النَّاسُ بِتَكْبِيرِهِمَا.
Imamu Bukhari (Rahimahullahu) amesema: 'Na alikuwa Ibn Umar na Abu Hurayrah (Allah Awe Radhi Nao) wakienda sokoni katika siku kumi (za Dhul Hijjah) wakileta Takbira (kwa sauti) na watu huleta Takbira kwa (kule kusikia) takbira za wawili hawa (yaani: Ibn Umar na Abu Hurayrah Allah Awe Radhi Nao)'.
Pia amesema kuwa:
وَكَانَ عُمَرُ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ يُكَبِّرُ فِي قُبَّتِهِ بِمِنًى فَيَسْمَعُهُ أَهْلُ الْمَسْجِدِ، فَيُكَبِّرُونَ وَيُكَبِّرُ أَهْلُ الأَسْوَاقِ، حَتَّى تَرْتَجَّ مِنًى تَكْبِيرًا.
'Na alikuwa Umar (Allah Awe Radhi Nae) akileta Takbira huku akiwa kwenye hema lake huko Mina, husikiwa na ahali wa Masjidi, basi (nao pia) huleta Takbira, na ahali wa maduka (pia huleta Takbira) hadi (kupelekea mji wa) Mina kutetemeka kwa Takbira.
' وَكَانَ ابْنُ عُمَرَ يُكَبِّرُ بِمِنًى تِلْكَ الأَيَّامَ وَخَلْفَ الصَّلَوَاتِ، وَعَلَى فِرَاشِهِ وَفِي فُسْطَاطِهِ، وَمَجْلِسِهِ وَمَمْشَاهُ تِلْكَ الأَيَّامَ جَمِيعًا.
'Na alikuwa Ibn Umar (Allah Awe Radhi Nao) akileta Takbira (nyakati zote) Mina katika siku hizo (za Tashriq), na (pia akileta Takbira) baada ya Sala (za Fardhi), na kitandani mwake, na katika hema lake, na majilisini mwake, na (katika) matembezi yake, huleta Takbira (katika) siku zote'.
Na inapendeza kujihirisha kwa Takbira kutokana na kitendo cha Umar, na Ibn wake, na Abu Hurayrah (Allah Awe Radhi Nao Jamia).Na inatupasa sisi Waislamu kuhuisha Sunnah hii iliyoadimika na kupotea (kufa) katika zama hizi, na inakaribia kusahauliwa hata na ahali wa swalaha (watendaji) mema na heri -kwa masikitiko makubwa - ni kinyume na walivyokuwa Salaf.
صيغة التكبير
Mfumo wa Uletaji wa Takbira
Katika kuleta Takbira kumepokelea namna nyingi kutokana na Swahaba (Allah Awe Radhi Nao Jamia) na Tabiina (Rahimahumullahu Jamia); miongoni mwake:
1.الله أكبر، الله أكبر، الله أكبر كبيرًا
2.الله أكبر، الله أكبر، لا إله إلاّ الله، والله أكبر، الله أكبر، ولله الحمد
3.الله أكبر، الله أكبر، الله أكبر، لا إله إلاّ الله، والله أكبر، الله أكبر، الله أكبر، ولله الحمد
صيام يوم عرفة
Kufunga Yawmu Arafah (Siku ya Arafa)
Kunasisitizwa na kutiliwa mkazo kufunga Yawmu Arafah (Siku ya Arafa) kutokana na yale yaliyothibiti kutokana na Rasuli wa Allah ﷺ kwamba amesema:
عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ "ِ صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ وَصِيَامُ يَوْمِ عَاشُورَاءَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ " .
Kutokana na Abu Qatadah (Allah Awe Radhi Nae) amesema kuwa: Rasuli wa Allah ﷺ amesema: “Saumu ya Siku ya Arafah nataraji kwa Allah kufuta (dhambi za) mwaka uliopita na (dhambi za) mwaka wa baada yake; na Saumu ya Ashuraa nataraji kwa Allah kufuta (dhambi za) mwaka uliopita.”
Lakini yeyote yule ambaye yuko Arafa -akiwa ni mwenye kuhiji- haipendezi kwake kufunga, kwa kuwa Nabii ﷺ alisimama Arafa hali ya kuwa hakufunga.
فضل يوم النحر
Fadhila za Yawmun Nahr (Siku ya Kuchinja)
Waislamu wengi hughafilika na Siku hiI adhimu Yawmun Nahr (Siku ya Kuchinja), (na hughafilika pia na) uadhama wa shani yake na utukufu wa fadhila zake nyingi na neema zake nyingi, hii ni pamoja na ukweli kwamba baadhi ya wanazuoni wanaona na kuamini kuwa Yawmun Nahr (Siku ya Kuchinja) ni siku bora zaidi ya mwaka, bila pingamizi.
Ibnul Qayyim (Rahimahullahu) amesema kuwa: 'Siku bora mbele ya Allah ni Yawmun Nahr (Siku ya Kuchinja), nayo ndio Siku ya Hajjil Akbar (Hijja kubwa kabisa) kama ilivyo katika Sunan Abu Dawud (Rahimahullahu).
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ قُرْطٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنِ النَّبِيِّ ﷺ قَالَ " إِنَّ أَعْظَمَ الأَيَّامِ عِنْدَ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى يَوْمُ النَّحْرِ ثُمَّ يَوْمُ الْقَرِّ " .
Kutokana na Abdullah bin Qurtwin (Allah Awe Radhi Nae) kutokana na Nabii ﷺ amesema: “Hakika Siku ziliyo bora (tukufu) kabisa kwa Allah (Tabaaraka wa Ta'alaa) ni Yawmun Nahr (Siku ya kuchinja), kisha Yawmul Qarri.” Na Yawmul Qarri ni ile siku ya kutulia Mina, nayo ni siku ya kumi na moja.
Na pamesemwa kuwa: Yawmu Arafah (Siku ya Arafa) ni bora kuliko hiyo (yaani: Yawmun Nahr), kwa kuwa Saumu yake inafidia (dhambi za) miaka miwili, na hakuna siku ambayo ndani yake Allah Anayoacha kwa wingi huru waja kutokana na Moto (wale waliostahiki kuingia Motoni) zaidi kuliko Yawmu Arafah (Siku ya Arafa), na kwamba Yeye (Subhaanahu wa Ta'alaa) katika (siku hiyo) Huwa karibu, kisha Hujigamba (yaani: kuhusu Ahali wa Kisimamo cha Arafah) kwa Malaika Wake.
Na kauli ya kwanza ndio sahihi; kwa kuwa Hadithi inadalilisha na kuthibitisha hilo na haipingwi na chochote.
Na ni sawasawa kama ikiwa Yawmun Nahr (Siku ya kuchinja) ndio siku bora au Yawmu Arafah (Siku ya Arafa ndio bora); kinachotakiwa na kutakikana kwa Muislamu -awe ni hajji (mwenye kuhiji) au mkaazi- kuwa mwangalifu ili apate kuweza kufikia kudiriki na kutambua fadhila zake na kuichangamkia fursa yake.
بماذا نستقبل مواسم الخير؟
Je, vipi tunatakiwa tuikaribishe misimu ya kheri?
1. Muislamu hutarajiwa na hutakiwa kupokea misimu ya kheri kwa Kuomba Tawbatan Nasuha (Tauba ya kwelikweli- ambayo inayojumuisha: kujiepusha na dhambi zote, kujuta, kuazimia kutorudia tena hiyo dhambi, kurudisha haki kwa aliyedhulumiwa, na iwe kwa gharadhi ya kutafuta Thawabu za Allah na Rehema Zake, na kuepuka -kukimbia- Adhabu na Ikabu Yake); yote kwa kuwa dhambi ndiyo inayomnyima na kumharamishia mja Fadhila za Rabi wake, na (pia hupelekea) kuwepo hijabu (kizuizi) moyoni mwake kunachombaidisha na Mola wake.
2. Kadhalika misimu ya kheri (kama hii na mengineyo) kwa ujumla hukaribishwa kwa dhamira na azimio la kweli na la dhati lenye kuthibitisha hamu na utayari wa mja wa kutaka kuitumia fursa itakiwavo na kumpelekea kuweza kufikia kufanya yale yenye Kuridhiwa na Allah; kwani yeyote yule mwenye kuwa mkweli na Allah, basi Allah Atamsadikisha.
وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ ﴿٦٩
﴾“Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, Tutawaongoza Sabili Zetu ...”
Ewe akh Muslim! Hakikisha unaitumia fursa hii vilivyo, kabla haijakupitia (utakuja) kujuta.
وفقني الله وإيَّاك لاغتنام مواسم الخير، وأن يعيننا فيها على طاعته وحسن عبادته
Namuomba Allah Aniwafikishe mimi na wewe katika kuweza kufaidika na misimu ya kheri, na Tunamuomba Atusaidie katika kuweza kufikia kumtii na kumuabudu uzuri wa kumuabudu kwenye misimu hii.
بعض أحكام الأضحية ومشروعيتها
Baadhi ya Hukumu za Udh hiyyah na Kuamrisha Kwake
Lililoasili kuhusu Udh hiyyah (kuchinja) ni kuwa ni haki waliyowekewa wale waliohai, kama alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allah ﷺ na Swahaba zake (Allah Awe Radhi Nao Jamia).
Walikuwa wakichinjia nafsi zao na ahali zao, ama kile ambacho baadhi ya watu wa kawaida (yaani: wasio kuwa na elimu) wanachodhania na kufikiria kuwa Udh hiyyah (kuchinja) ni mahususi kwa wafu, basi (ni vyema tuelewe kuwa) hili halina msingi wowote ule katika Dini.
Udh hiyyah kwa niaba ya kuwachinjia wafu imegawanywa katika vigawanyo vitatu:
Cha kwanza: Kuwachinjia wafu kwa niaba yao kwa kuwajumuisha na waliohai
Mfano mtu anajichinjia (nafsi yake) na (hapohapo) anachinjia ahali baiti yake, na katika dhamira yake (anakusudia) kuwajumuisha waliohai na wafu, na asili ya hii ni uchinjaji wa Nabii ﷺ kwa nafsi yake na ahali baiti yake na miongoni mwao walikuwemo waliokuwa wameshakufa kabla.
Cha pili: Kuwachinjia wafu kwa ajili ya kutekekeza wasia wao.
Na asili ya hii ni Kauli Yake Ta’alaa:
فَمَن بَدَّلَهُ بَعْدَ مَا سَمِعَهُ فَإِنَّمَا إِثْمُهُ عَلَى الَّذِينَ يُبَدِّلُونَهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٨١
﴾ "Atakayeubadilisha (wasia) baada ya kuusikia, basi hakika dhambi yake ni juu ya wale watakaoubadilisha; hakika Allah ni Samiy'un (Mwenye Kusikia yote) Alimu."
Cha tatu: Kuwachinjia wafu pekee (bila ya kuwajumuisha na waliohai) kwa kujitolea, hii inajuzu.
Na Fuqahaa wa dhehebu la Kihanbali wameeleza kuwa thawabu zake zinamfikia maiti na ananufaika nazo (kauli yao hii inaegemezwa na) Qiyaas ya kumtolea (maiti) sadaka kwa niaba yake, lakini hatuoni (usahihi wa) kumchinjia maiti mahususi (hususan bila ya kumjumuisha na waliohai) ni katika Sunnah, kwa kuwa Nabiiﷺ hakumchinjia mmoja yeyote yule mahususi (hususan bila ya kumjumuisha na waliohai) katika maiti zake.
Nabiiﷺ hakumchinjia ami yake Hamza (Allah Awe Radhi Nae), ambaye alikuwa mmoja wa jamaa zake wa karibu na kipenzi, na wala (hakuwachinjia) mahususi (hususan bila ya kuwajumuisha na waliohai) waladi zake ambao walikufa wakati wa uhai wakeﷺ, ambao ni mabanati watatu waliokuwa wamekwishaolewa (Allah Awe Radhi Nao Jamia) na wala (hakumchinjia) zaujiti wake Khadija (Allah Awe Radhi Nae), ambaye ndie kipenzi zaidi katika wake zake wote (Allah Awe Radhi Nao Jamia), na wala haikupokelewa kutokana na Swahaba (Allah Awe Radhi Nao Jamia) katika zama zake ﷺ kwamba mmoja yeyote yule aliwahi kumchinjia yeyote yule katika maiti zake.
•Na pia tunaona kuwa katika makosa ambayo yanafanywa na baadhi ya watu, kumchinjia maiti mwaka wake wa kwanza anapofariki kichinjo kinachoitwa أضحية الحفرة (dhabihu ya shimo), wanaitakidi kuwa haijuzu kwa mmoja yeyote yule kushirikiana naye katika thawabu zake (kichinjo cha shimo), au huwachinjia maiti wao kwa kujitolea (kwa hiari yao), au kutokana na wasia zao, (na kinachosikitisha ni) kuwa hawajichinjii nafsi zao na familia zao, lau wangelielewa kuwa kama mtu anajichinjia nafsi yake na ahali zake kutokana na mali yake huwa inawajumuisha pamoja ahali zake waliohai na wafu, basi wasingelikengeuka kufanya hivyo.
فيما يجتنبه من أراد الأضحية
Yale Anayotakiwa Kujiepusha Nayo Mwenye Kutaka Kuchinja
Mwenye kudhamiria kuchinja na ikawa shahari ya Dhul Hijjah umeingia: ima kwa kuona hilali au kukamilisha siku thelathini za Dhua Qa'dah basi ni haitakikani (Sh. katumia tamshi: haramu) kwake kunyoa (kukata) chochote kile katika nywele zake au kuchuna ngozi ya mwili wake mpaka achinje kichinjo chake, kutokana na Hadithi ya Ummu Salamah
عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ رضي الله عنها أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ قَالَ :" إِذَا رَأَيْتُمْ هِلاَلَ ذِي الْحِجَّةِ وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ فَلْيُمْسِكْ عَنْ شَعْرِهِ وَأَظْفَارِهِ
Kutokana na Ummu Salamah (Allah Awe Radhi Nae) kwamba Nabii ﷺ amesema: “Mtakapouona mwezi wa Dhul Hijjah na mmoja wenu akadhamiria kuchinja, basi ajizuie (kukata) nywele zake na kucha zake.” Na katika lafdhi:
" فَلاَ يَأْخُذَنَّ مِنْ شَعْرِهِ وَلاَ مِنْ أَظْفَارِهِ شَيْئًا حَتَّى يُضَحِّيَ "
“Basi asiguse (asikata) chochote kile katika nywele zake na wala katika kucha zake mpaka atakapochinja.”
Na kama atadhamiria kuchinja katika siku kumi (mfano siku pili au ya tatu na kadhallika), basi atatakiwa ajiepushe (na hayo yaliyokatazwa) kuanzia pale alipodhamiria, na hakuna dhambi kama atakuwa amekata (nywele au kucha) kabla ya huko kudhamiria kwake.
والحكمة في هذا النَّهي
Hekima katika katazo hili Ni kuwa:
Pale mwenye kuchinja aliposhirikiana na mwenye kuhiji katika baadhi ya amali za ibada ya Hijjah, ambazo ni (miongoni mwa amali za) kujikurubisha kwa Allah kwa kule kuchinja kwake kichinjo, basi hushirikiana nae (pia) katika baadhi ya sifa maalumu za Ihramu katika kujizuia (kukata) nywele na mfano wa hayo, na hivyo basi inajuzu kwa ahali wa mwenye kuchinja (yaani: sio mchinjaji mwenyewe) kukata nywele zao, kucha zao na kuchukua chochote kile katika miili yao katika hizo siku kumi.*
Hukumu hii (ya kujizuia kukata nywele na mfano wake) ni mahususi kwa yule anayechinja, ama yule anayechinjiwa (ahali wa mchinjaji na kadhalika) huwa haimhusu; kwa kuwa Nabii ﷺ kasema:
"وَأَرَادَ أَحَدُكُمْ أَنْ يُضَحِّيَ. "
"Na mmoja wenu akadhamiria kuchinja ...”
Na wala hakusema au anayechinjiwa (ahali wa mchinjaji na kadhalika); na kwa sababu Nabii ﷺ alikuwa akichinja kwa niaba ya ahali zake, na haikupokelewa kutokana nae ﷺ kwamba aliwaamrisha (ahali zake) kujizuia (kukata) nywele na mfano wa hayo.
Na mwenye kudhamiria kuchinja akikata chochote kile katika nywele zake, au kucha zake au mwili wake, basi ni lazima atubie kwa Allah, na wala asirudie (asifanye tena), na wala hana kafara, na hilo halimzuii kuchinja kama wanavyodhania baadhi ya watu wa kawaida.
Na pale atakapokata chochote kile katika hayo hali ya kusahau au kutojua, au nywele zimedondoka (anguka) bila kukusudia, basi hakuna dhambi juu yake, na wakati wowote ule akihitaji kukata (nywele zake na mfano wa hayo) basi anaweza kukata, na wala hakuna ubaya wowote ule juu yake, mfano kucha yake imekatika na inamuudhi (inamuumiza) basi anaweza kuukata, au nywele zinamuudhi (zinashuka na kuingia) machoni mwake, basi anaweza kuzikata, au anahitaji kuzikata kwa gharadhi ya kutibu jeraha na kadhalika.
أحكام وآداب عيد الأضحى المبارك
Akh habibi ….. Tunakusalimu kwa salamu ya Kiislamu - kwa kusema:
السلام عليكم ورحمة الله وبركاته
Na tunakupongeza mapema kwa ujio wa Idil Adh-haal Mubaarak, na kwa kusema:
تَقَبَّلُ اللهُ مِنٌّا وَمِنْكُم
Allah Atutakabalie (amali njema) kutoka kwetu na kutoka kwako,
Na (pia) tunatarajia na kutumainia kuwa utaikubali kutoka kwetu risala hii, ambayo tunamuomba Allah iwe na manufaa kwako na kwa Waislamu jamia wa kila pahala.
Ewe Akh wangu Muislamu! Kheri yote inapatikana katika kufuata (na kushikamana na) Uongofu wa Nabiiﷺ katika kila jambo la maisha yetu, na shari yote hupatikana katika kuhalifu Uongofu wa Nabii wetuﷺ , hivyo basi, tunapenda kukumbushana baadhi ya mambo yanayopendeza (na kutakikana) kufanywa au kusemwa katika usiku wa Idil Adhhaal Mubaarak na Yawmun Nahr, na siku tatu za Tashriq, na tumekufupishia kwa muhtasari katika nukta zifuatazo:
التكبير
Takbira: Hutakiwa kuletwa huanzia Alfajiri ya siku ya Arafa hadi Alasiri ya siku ya mwisho ya Tashriq, ambayo ni (siku ya) kumi na tatu ya mwezi wa Dhul Hijjah,
Allah Amesema:
وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ .. ﴿٢٨
﴾“Na wadhukuru (wataje) Jina la Allah katika masiku yanayojulikana….”
Na wasifu wake ni kusema:
الله أكبر، الله أكبر، لا إله إلاّ الله، والله أكبر، الله أكبر، ولله الحمد
Na inasuniwa (ni Sunnah) kwa wanaume kuijihirisha (hiyo Takbira) misikitini, na masokoni na majumbani, na baada ya Sala, kuonyesha Uadhimu na Utukufu wa Allah na kudhihirisha kumuabudu kwake na kumshukuru.
* ذبح الأضحية
Kuchinja Udh hiyyah: Hutakikana kufanyike baada ya Sala ya Idi, kwa mujibu wa kauli ya Rasuli wa Allah
:"مَنْ ذَبَحَ قَبْلَ أَنْ يُصَلِّيَ فَلْيُعِدْ مَكَانَهَا أُخْرَى، وَمَنْ لَمْ يَذْبَحْ فَلْيَذْبَحْ "
.
“Aliyechinja kabla ya kuswali (Sala ya Idi), basi achinje kichinjo chengine badala yake; na yule ambaye bado hajachinja, basi na achinje.”
Na muda wa kuchinja ni siku nne: Yawmun Nahr, na siku tatu za Tashriq, kutokana na yale yaliyothibitika kutokana na Nabii ﷺ kuwa amesema:
" وكل أيام التشريق ذبح.
"“Na siku zote za Tashriq huchinjwa"
الاغتسال والتطيب للرجال
Kukoga na (kujitia) manukato kwa Wanaume:
Kuvaa nguo nzuri bila isirafu na bila ya isibali (kuburuza nguo), na bila ya kunyoa ndevu hili ni haramu.Ama wanawake wanatakikana kwenda kwenye musalla (sehemu inayosaliwa Sala ya) Idi bila ya kujishaua na kujipamba na bila ya kujitia manukato, haifai kwao kwenda kumtii Allah kwa kusali kisha wanamuasi Allah kwa kujishaua, kujifunua na kujitia manukato (huku) wakiwa mbele ya wanaume.
الأكل من الأضحية
Kula kutokana na Udh hiyyah:
Alikuwa Rasuli wa Allah ﷺ hali (kitu) mpaka arudi kutoka kwenye musalla basi (anaporudi) ndio hula, tena hula kutokana na udh hiyyah yake.
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بُرَيْدَةَ، عَنْ أَبِيهِ رضي الله عنهما قَالَ كَانَ النَّبِيُّ ﷺ لاَ يَخْرُجُ يَوْمَ الْفِطْرِ حَتَّى يَطْعَمَ وَلاَ يَطْعَمُ يَوْمَ الأَضْحَى حَتَّى يُصَلِّيَ .
Kutokana na Abdillah bin Buraydah kutokana na baba yake (Allah Awe Radhi Nao) amesema kuwa: ‘Alikuwa Nabii ﷺ hatoki Siku ya Fitri (kwenda kusali Sala ya Idil Fitr) mpaka ale (tende witiri), na wala hali (chochote kile) Siku ya Idil Adh haa mpaka asali (Sala ya Idil Adh haa).‘ Huu ndio Uongofu wa Nabiiﷺ kuhusiana na Siku ya Idil Adh haa kwamba hali mpaka arudi kutoka kwenye musalla.
الذهاب إلى مصلى العيد ماشياً إن تيسر
Kwenda kwenye Musalla wa Idi kwa miguu ikiwezekana (na hili ndio bora):
Ni (katika) Sunnah kuisali (Sala ya Idi) kwenye musalla wa Sala ya Idi isipokuwa kama kutakuwa na udhuru kama vile mvua kwa mfano, basi itasaliwa msikitini kutokana na kitendo cha Rasuli wa Allah ﷺ.*الصلاة مع المسلمين
واستحباب حضور الخطبة
Kusali pamoja na Waislamu, na inapendeza kuhudhuria (kusikiliza) hutuba:
Na kile ambacho kimependelewa na chenye nguvu kwa wanazuoni mithili Shaykhul Islam Ibn Taymiyyah (Rahimahullahu) ni kwamba: Sala ya Idi ni wajibu kutokana na Kauli Yake Allah:
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ
﴿٢﴾“Basi sali kwa ajili ya Rabi wako na chinja.
” Na (Sala ya Idi) haiporomoki isipokuwa kwa udhuru, na wanawake wanatakiwa kuhudhuria (Sala ya Idi) pamoja na Waislamu hata walio kwenye siku zao (hedhi) na wazee vikongwe, na walio kwenye siku zao kubaki mbali (kujitenga) na musalla.
مُخَالَفَة الطريق
Kubadili Tarika (njia):
Inapendekezwa kwako kwenda kwenye musalla wa Idi kwa kutumia tarika moja na kurudi kwa kutumia tarika nyengine kutokana na kitendo cha Nabii wa Allah
التهنئة بالعيد
Kupongezana kwa ajili ya Sikukuu:
Kwa kule kuthibiti hilo kutokana na Swahaba wa Rasuli wa Allahﷺ
.واحذر أخي المسلم من الوقوع في بعض الأخطاء التي يقع فيها الكثير من الناس والتي منها
Jihadhari akh yangu Muislamu usije ukatumbukia katika baadhi ya makosa ambayo hufanywa na watu wengi yakiwemo:
التكبير الجماعي بصوت واحد
Kuleta Takbira kwa pamoja kwa sauti moja, au kumuitika (kuisoma baada ya kusomwa na) mwenye (kuongoza) katika uletaji wa Takbira.
اللهو أيام العيد بالمحرمات
Kujiburudika siku za Idi kwa mambo (au vitu) vilivyoharamishwa (katazwa),
Kama vile kusikiliza nyimbo, kushuhudia na kutazama mafilamu (sinema zisizo na maadili yenye kwenda sambamba na Uislamu), wanaume kuchanganyika na wanawake ambao si maharimu zao, na yasiyokuwa hayo katika matendo au mambo ya munkari.
أخذ شيء من الشعر أو تقليم الأظافر قبل أن يُضحي
Kukata (chochote kile) katika nywele au kukata (kupunguza) kucha kabla ya kuchinja (kwa aliyedhamiri kuchinja), kwa sababu Rasuli wa Allahﷺ amelikataza hilo.
الإسراف والتبذير
Isirafu na ubadhirifuKufanya isirafu na ubadhirifu kwa mambo ambayo hayana maslahi wala manufaa;
Kwa mujibu wa Kauli Yake Ta'alaa:
وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿
١٤١﴾"Na wala msifanye isirafu; hakika Yeye (Muumba) Hapendi wafanyao isirafu."
Hitimisho:
Ewe akh yangu Muislamu! Usisahau kujitahidi kutenda amali njema na za kheri, kama vile kuunga udugu na kuzuru jamaa na kuacha kubughudhiana, na husuda, na kuchukiana, na kujitahidi kuutakasa moyo kutoka na hayo, (kujitahidi) kuwa mpole na kuwafanyia ihsani masikini, na mafukara, na mayatima, na kuwasaidia.
نسأل الله أن يوفقنا لما يحب ويرضى، وأن يفقهنا في ديننا ، وأن يجعلنا ممن عمل في هذه الأيام أيام عشر ذي الحجة عملاً صالحاً لوجهه الكريم
Tunamuomba Allah Atuwafikishe kwa yale Anayoyapenda na Kuyaridhia, na (Atufanyie wepesi) kuifahamu Dini yetu, na Atujaalie tuwe miongoni mwa wale waliotenda amali njema katika Siku Kumi hizi za Dhul -Hijjah kwa ajili ya Wajihi Wake Karimu.