top of page

Asmaaul Llaahil Husnaa

 

Abu ‘Ammaar, Abdulrazak Kombo Khiari

 

Moja katika mambo muhimu ya kimsingi kwa kila Muislamu ni kumjua anaemuabudu. Tukimjua tunaemuabudu tutaweza kumuabudu kiukweli, kwa dhati na kumpa kila haki anayostahiki kwani tutakuwa tumefahamu vyema wajibu wetu kwake na jinsi ya kumuabudu.

 

Pale ambapo mja atajihimu na kujifunza ili amjue anaemuabudu basi atakuwa anafanya jambo muhimu ambalo kwa ajili yake Allaah Subhaanahu Wata’ala amemuumba.

 

Na endapo kama atalidharau na kutolipa umuhimu jambo hili basi atakuwa analiwacha jambo ambalo kwa kwa ajili yake Allaah Subhaanahu Wata’ala amemuumba.

 

Malengo ya kuyajua na kuyafahamu majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala pamoja na sifa zake ni kuweza kuwa na elimu na kufahamu maana zake na kisha kuweza kuyafanyia kazi kwani miongoni mwa majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala pamoja na sifa zake ni yale ambayo hata mja anaweza kuwa na sifa hizo kama sifa ya kuwa na elimu, sifa ya kuwa mwenye kuwaonea huruma watu au kuwa na sifa ya uadilifu.

 

Lakini kuna majina na sifa za Allaah Subhaanahu Wata’ala ambayo hapaswi mja kuwa na sifa ya Uungu, sifa ya Jabbaar (kufanya alitakalo) sifa ya kuwa na kiburi kwani hizi ni sifa na majina maalum kwa Allaah Subhaanahu Wata’ala pekee.

 

Allaah Subhaanahu Wata’ala amesema: Hakika Allaah ana majina yaliyo bora basi muombeni kwa majina yake. Al A’raaf 180

 

Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amesema: Hakika Allaah Subhaanahu Wata’ala ana majina 99, majina mia isipokuwa moja tu. Mwenye kuyahesabu vizuri basi ataingia peponi. (Muttafaqun ‘Alayhi)

Historia ya Majina ya Allah Subhaanahu Wata’ala

 

Jambo lililothibiti na ambalo halina shaka ni kwamba Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amethibitisha kwamba Allaah Subhaanahu wata’ala ana majina 99 kama ilivyopokewa kwenye hadithi aliyosimulia Abu Hurayrah, radhiya Llaahu ‘anhu.

 

Hata hivyo hakuna uthibitisho wowote kwamba Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam aliyataja majina yenyewe. Hakuna hadithi au riwaya yoyote iliyothibiti kutoka kwa Mtume Swalla Alaahu ‘alayhi wasallam yenye kuthibitisha kutajwa majina haya.

 

Hivyo majina haya yalipatikana vipi?

 

 

Mwishoni mwa karne ya pili Hijriya na mwanzoni mwa karne ya tatu walitokea wapokezi wa hadithi ambao walijaribu kuyakusanya majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala.

 

Vigezo walivyotumia ni kuyatoa katika Qur’aan, mengine kutoka katika Sunna na mengine kwa mujibu wa kujitahidi kwao na kufuata ijtihad za wanazuoni waliokuwepo katika wakati wao.

 

Mpokezi wa mwanzo kuifanya kazi hii alikuwa ni Al Walid bin Muslim. Alifuatiwa na Abdulmalik As San’aani. Wa mwisho alikuwa Fahd Abdulaziz bin Husayn.Wapokezi hawa watatu walijitahidi kuyakusanya majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala na kila mmoja wao aliweza kufikisha majina 99.

 

Naam walifanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano kwani waliweza kufikiria jambo ambalo hadi hivi leo, na nnaamini hadi siku ya kiama, majina haya yataendelea kutumika na kutajwa. Allaah Subhaanahu Waata’aala awape Tawfiyq na awawafikishe kwa jitihada yao kubwa. Amin

 

Hata hivyo majina aliyokusanya Al Walid bin Muslim ndiyo yaliyokuwa mashuhuri zaidi kwa takriban miaka 1000. Majina haya ndiyo huyaona sana kwenye picha au hata katika mitandao na wengine wakifikiri labda yanatokana na hadithi ya Mtume swalla Allaahu ‘alayhi wasallam kutokana na umashuhuri wake.

 

 

Tunapenda ifahamike vizuri kwamba majina haya licha ya umashuhuri wake ni vyema yakafahamika kwamba si miongoni mwa hadithi za Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam zilizothibiti bali ni ijtihaad ya wapokezi wa hadithi ambao ni miongoni mwa Taabii Taabiin yaani wale waliofuatia baada ya Masahaba na Taabiin.

 

Maulamaa wamewafikiana kwamba katika kuyatambua majina ya Allaah lazima tutosheke na yale tu yaliyothibiti ima katika Qur’aan au katika Sunna sahihi za Mtume Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam bila ya kuongeza au kupunguza jina lolote.

 

Kwa hivyo jitihada yoyote itakayofanyika lazima ikidhi vigezo hivi muhimu kwani hatuwezi kutumia rai au akili zetu katika jambo ambalo akili haina uwezo huo wa kuweza kuyatambua na kuyabaini majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala.

 

Hivyo ni lazima na ni muhimu kwa kila jina liwe na dalili iliyothibiti ili tuweze kulikubali jina hilo pasi na shaka yoyote kwamba ni jina la Allaah Subhaanahu Wata’ala.

 

Vyenginevyo kama jina hilo halikuthibiti katika Qur’aan au katika Sunna sahihi basi itakuwa ni Ijtihaad. Na Maulamaa tayari wamekubaliana kutoruhusu kutumika Ijtihaad katika kuyatambua na kuyabaini majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala.

 

Maulamaa wamefafanua kwamba kuyahesabu majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala kunamaanisha yafuatayo:

 

1       Kuweza kuyahesabu majina na kujua matamshi yake.

2       Kufahamu maana zake, makusudio yake na kuyaamini.

3       Kumuomba Allaah Subhaanahu Wata’ala kwa kutumia majina na sifa zake.

 

Majina ya Allaah yanaashiria dhati ya Allaah Subhaanahu Wata’ala ambayo imesifika kwa sifa zote za ukamilifu.

 

Hakika kila jina la Allaah Subhaanahu Wata’ala lina maana kubwa inayoonesha uwezo wa Allaah Subhaanahu Wata’ala na ukamilifu wake.

 

Yafuatayo ni majina ya Allaah Subhaanahu Wata’ala pamoja na maana zake na dalili ya kuthibiti kwake

    
Jina            Jina ( Kiarabu)    Maana kwa kiswahili    Maelezo     Dalili
   Allaah            اللَّهُ                         Mwenyezi Mungu    Mwenye haki ya Uungu, mwenye haki ya kuabudiwa na waja wake wote. Yeye ndie mwenye haki ya kuabudiwa, kunyenyekewa, kusujudiwa na kuabudiwa kwa aina zote za ibada    
1    Ar Rahmaan    الرَّحْمَنُ    Mwenye Rehma    Ni jina linalothibitisha jinsi rehma zake zilivyoenea na kusambaa kwa waja wake wote. Jina hili ni maalum kwa Allaah Subhaanahu Wata’ala pekee na haipasi mtu yeyote au kiumbe chochote kujipa jina hili kama lilivyo.    Fussilat 2
تَنْزِيلٌ مِنَ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
2    Ar Rahim    لرَّحِيمُ ا    Mwingi wa kurehemu    Mwenye kuwarehemu waumini duniani na kesho akhera. Amewaongoa duniani kwa kumuabudu yeye pekee, atawakirimu kesho akhera kwa pepo yake.    Fussilat 2
تَنْزِيلٌ مِنَ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ
Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu
3    Al ‘Afuww    العَفُوٌّ    Mwenye kusamehe    Mwenye kusamehe madhambi na kuyafuta kabisa na kutoadhibiwa kwa mja licha ya kustahiki adhabu.    An Nisaa 149
فَإِنَّ اللهَ كَانَ عَفُوّاً قَدِيراً
Hakika Allaah ni Mwingi wa maghfira na Muweza.
4    Al Ghafuur    الْغَفُورُ    Mwenye kusamehe    Mwenye kusitiri dhambi za waja, wala hamfedheheshi mja kwa dhambi zake na pia humsamehe makosa yake    Al Buruuj 14
وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُود
Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi
 

WELCOME

bottom of page